Raila Afichua Kiongozi Mkuu Wa Mashambulizi Dhidi Ya Wafuasi Wa Azimio Huko Kisii
Kiongozi wa chama cha Azimio la Umoja One-Kenya Raila Odinga amelaumu baadhi ya wafuasi wa Muungano wa kenya kwanza kwa kuandaa machafuko yaliyokumba mkutano wa kuipinga serikali katika Kaunti ya Kisii mnamo Ijumaa, Februari 17.
Katika taarifa iliyotolewa, Raila amedai kuwa baadhi ya wanasiasa wa UDA walifanya kazi na genge la wahalifu kuwavamia wafuasi wake na hivyo kusababisha mashambulizi katika mkutano huo.
Aidha amebainisha kuwa mashambulizi yaliongozwa na mhalifu ambaye alikuwa na vibali kadhaa vya kukamatwa kwa jina lake.
Raila, ambaye alikosa kumtaja kiongozi huyo wa serikali, amebainisha kuwa mashambulizi hayo yanaashiria juhudi za serikali kuingiza nchi katika machafuko.
Kiongozi huyo wa chama cha ODM ametoa wito kwa wanasiasa kuelekeza mawazo yao kwake na wala si wafuasi wake- ambao alisema walikuwa wakilengwa kwa nia ya kuhudhuria mkutano wake.
Kauli ya Raila inajiri baada ya makabiliano kati ya wafuasi wa Azimio la Umoja na Kenya Kwanza mjini Kisii kushuhudiwa.
Ripoti zilionyesha kuwa vijana kadhaa waliwarushia mawe wafuasi wa Kenya Kwanza waliokuwa na maandamano karibu na Hospitali ya Ram kando ya njia ya Daraja Moja-Nyamataro.
Akilaani tukio hilo katika eneo la tukio, kiongozi wa kundi la United Democratic Alliance (UDA) Fred Nunda alisema walikuwa wakifanya maandamano ya amani kabla ya kuchokozwa na wapinzani wao.