Home » ODM Yataka Mbunge Wa Gem Elisha Odhiambo Kufurushwa Kutoka Chamani

ODM Yataka Mbunge Wa Gem Elisha Odhiambo Kufurushwa Kutoka Chamani

Mbunge wa Gem Elisha Odhiambo leo amekuwa mbunge wa pili wa Siaya kukabiliwa na vitisho vya kufukuzwa kutoka chama cha (ODM) baada ya tawi la Gem ODM kupendekeza atimuliwe kufuatia ziara yake Ikulu wiki mbili zilizopita.

 

Huku wito wa kuwatimuliwa kwa wanaodaiwa kuwa wabunge walioasi wa ODM ukishika kasi, kikao cha kamati kuu ya tawi la Gem ODM kilichofanyika katika kituo cha biashara cha Sagam kimeshinikiza kumtimua mbunge huyo na baadhi ya washirika wake kutoka nyadhifa zilizokuwa katika tawi hilo, ambapo Odhiambo alikuwa mwakilishi wa chama hicho maalum.

 

Akihutubia wanahabari baada ya mkutano huo, mwenyekiti wa tawi hilo Nick Ochola amesema kuwa mbunge huyo na mmoja wa wanachama wa kamati kuu ya tawi John Ogam Maramba wamekuwa wakifanya kazi kwa maslahi ya wapinzani wa ODM na wamefanya kampeni dhidi ya wagombeaji wa ODM katika uchaguzi mkuu uliopita.

 

Aidha amesema kuwa wawili hao walikuwa pamoja tena wakati wa uchaguzi mdogo wa Desemba 8, 2022 katika wadi ya Gem kusini ambapo walifanya kampeni za wazi dhidi ya mgombea mteule wa ODM Polycarp Wanga ambaye alishindwa na mgombeaji huru.

 

Mbunge huyo ameshutumiwa zaidi kwa kutetea maslahi na sera za vyama pinzani kwa kukutana na uongozi wa Muungano wa Kenya kwanza katika Ikulu ya Nairobi mnamo 7/2/2023 na hivyo kukiuka katiba ya ODM.

 

Mwenyekiti wa kamati ya kuratibu ya chama kaunti ya Siaya Oloo Okanda naye amepongeza uamuzi wa Tawi la Gem, akiongeza kwamba chama lazima kiondoe watu ambao si waaminifu.

 

Odhiambo anakuwa mbunge wa pili kutoka Kaunti ya Siaya kukabiliwa na vitisho vya kufurushwa kutoka kwa chama hicho baada ya ODM tawi la Bondo pia kumsimamisha kazi mbunge Gideon Ochanda kutoka chama hicho na kumwondolea majukumu yake kama katibu wa tawi mapema wiki hii.

 

Iwapo watafukuzwa katika chama, wawili hao wana hatari ya kupoteza viti vyao vya ubunge.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!