Azimio Yaahirisha Mkutano Wa Kisii
Muungano wa Azimio la Umoja umeahirisha mkutano wake mkuu uliokuwa ufanyike katika uwanja wa Gusii leo hii Jumatatu.
Kulingana na Mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Kisii, Kerosi Ondieki, mkutano huo uliopangwa umesogezwa hadi Ijumaa, Februari 17 ili kutoa nafasi kwa maandalizi ifaayo.
Mwenyekiti wa Kaunti pia amesema waliomba usamamizi wa Azimio kumwezesha Gavana wa Kaunti Simba Arati kuongoza mipango ifaayo ya kuingia kwake katika uwanja wa Gusii.
Matukio hayo yanafuatia maandamano ya viongozi wa Kisii wanaoegemea upande wa Rais William Ruto, ambaye Jumapili alidai Azimio kusitisha mikutano yao akisema hawakukaribishwa Kisii.
Sasa, Kerosi ametaja matamshi yaliyotolewa na aliyekuwa Gavana wa Kisii James Ongwae na Joash Maangi kuwa ya kejeli, akitaka wakazi wajitokeze kwa wingi kukaribisha kikosi cha Azimio ndani ya uwanja huo wa kihistoria mnamo Ijumaa.
ODM inashikilia kuwa bado wako sawa katika eneo kubwa la Gusii na hawatawahi kukatishwa tamaa na hisia za watu wanaogombania nyadhifa chini ya Utawala wa Kenya Kwanza.