Home » Wabunge Wa Jubilee Wajitolea Kufanya Kazi Na Rais Ruto Baada Ya Mkutano Wa Ikulu

Wabunge Wa Jubilee Wajitolea Kufanya Kazi Na Rais Ruto Baada Ya Mkutano Wa Ikulu

Rais William Ruto asubuhi ya leo amekutana na kundi la takriban wabunge 30 wa chama cha Jubilee katika Ikulu ya Nairobi.

 

Hii ikiwa ni mara ya pili kwa timu hiyo kukutana na Rais Ruto, wamejitolea kufanya kazi na serikali tawala ya Kenya kwanza.

 

Baadhi ya wanachama waliohudhuria ni Mbunge wa Eldas Aden Keynan, John Waluke wa (Sirisia), Mark Mwenje wa (Embakasi Magharibi), mbunge mteule Sabina Chege, Stanley Muthama wa (Lamu Magharibi) na Yusuf Hassan wa (Kamukunji) miongoni mwa wengine mkutano ambao Naibu Rais Rigathi Gachagua pia alikuwepo.

 

Haya yanajiri saa chache baada ya mkutano kati ya Mkuu wa Nchi na baadhi ya wabunge kutoka chama cha upinzani cha (ODM), kufanyika jana katika msingi uo huo, ambao umezua mvutano ndani ya chama hicho.

 

ODM, kupitia Mkurugenzi wake wa Mawasiliano Phillip Etale, imesema ziara ya wabunge hao Ikulu haikushangaza kwa sababu baadhi yao walikuwa wakifuatiliwa katika maandalizi ya ziara hiyo.

 

Chama hicho hata hivyo kimewataka Wakenya kuwapuuza viongozi hao kwa kuwashutumu kwa ubinafsi na kuongozwa na maslahi yao kwa gharama ya mamilioni ya Wakenya maskini.

 

Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwour almaarufu Jalang’o, ambaye alikuwa sehemu ya timu iliyolaaniwa, alifafanua kuwa mkutano huo ulikuwa wa maendeleo wala si wa kisiasa.

 

Wakati huo huo muungano wa Azimio la Umoja umeitisha mkutano wa lazima wa wajumbe wa Bunge lao Alhamisi wiki hii, ambapo wanatishia kuchukua hatua za kinidhamu kwa wanachama wasio waaminifu.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!