Home » Seneti Yachukua Hatua Kusuluhisha Mizozo Inayoibuka Katika Kaunti

Seneti Yachukua Hatua Kusuluhisha Mizozo Inayoibuka Katika Kaunti

Bunge la Seneti limebainisha mzozo kati ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kuwa baadhi ya mizozo inalopanga kutatua siku zijazo.

 

Kupitia kwa Kamati ya Ugatuzi, imebainisha Kiambu, Kericho, Kisii, Migori na Busia kuwa baadhi ya kaunti zinazokabiliwa na mizozo kati ya Utendaji na Mabunge ya Kaunti.

Haya yanajiri huku kamati hiyo ikieleza wasiwasi wake kuhusu miswada inayosubiriwa ambayo ilikuwa ikiathiri imani ya wawekezaji.
Katika wiki kadhaa zilizopita, wawakilishi wadi katika kaunti zilizoorodheshwa wametofautiana na watendaji hao kuathiri vibaya utoaji wa huduma.

Kulingana na mwenyekiti wa kamati hiyo Mohammed Abass, mizozo inayoongezeka ilikuwa ikiathiri ari ya ugatuzi na kusema kuwa kamati hiyo itazuru kaunti zote zilizoathiriwa ili kufahamu tatizo hilo na njia ya kusonga mbele.

Abass amesema kuwa wamefaulu kuzuru kaunti za Meru na Tharaka Nithi ambapo tofauti za uongozi na mipaka mtawalia zilikuwa zimetatuliwa.

 

Seneta wa Wajir Ali Abdullahi Ibrahim wakati uo huo ameelezea wasiwasi wa kamati kuhusu miswada ambayo haijashughulikiwa akibainisha kuwa hii inaweza kulemaza utoaji wa huduma.

 

Aidha ameelekeza Nairobi na Wajir ambako bili mbalimbali zilizokuwa hazijakamilika zimefikia shilingi bilioni mia 100 na shilingi bilioni 5 mtawalia, akitaja takwimu hizo kuwa nyingi na zenye kutiliwa shaka.

 

Vile vile ameshangaa jinsi takwimu hizo zilivyopanda hadi viwango vya sasa ilhali kaunti zilikuwa zimezipangia bajeti lakini wanakandarasi walikuwa hawajalipwa kwa miaka mingi.

 

Kwa upande wake, makamu mwenyekiti wa kamati Catherine Muma, amekaribisha mkutano uliopangwa wa naibu rais Rigathi Gachagua na viongozi waliochaguliwa wa Meru.

 

Seneta huyo aliyeteuliwa aliongeza kuwa bili zinazosubiriwa zinapunguza imani ya wawekezaji akibainisha kuwa mamia ya wafanyabiashara wamepoteza pesa zao walizochuma kwa bidii.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!