Wasanii wa Injili Wachangisha Pesa Kumjengea Nyumba Ilagosa Wa Ilagosa

Wasanii wa nyimbo za Injili na Marafiki wa mwimbaji wa nyimbo za Injili marehemu Ilagosa Wa Ilagosa wamechangisha fedha ili kumjengea nyumba kijijini hapo.
Kulingana na mila za Waluhya, Ilagosa Wa Ilagosa atalala ndani ya nyumba hiyo akisubiri mazishi baada ya mwili kuhamishwa kutoka chumba cha maiti. Mazishi yamepangwa tarehe 16 Februari 2023.
Vikundi viwili vya WhatsApp vimeundwa kusaidia katika kuchangisha fedha, vyote vina zaidi ya watu 1,500. Vyanzo vya karibu vimefichua kuwa makadirio ya bajeti ya ibada ya mazishi ya Ilagosa ni takriban KSh M1.5. Kufikia sasa, wamechangia Ksh 300,000 kwa mpango huo.
Msanii huyo wa wimbo wa ‘sala zangu’ alifariki siku ya Ijumaa alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali moja huko Langata.
Chanzo cha kifo hicho hakijafichuka hata hivyo video yake akidai mtu alikuwa akipanga kukatisha maisha yake imesambaa mitandaoni.
Katika video hiyo Illagosa anadai kwamba mtu fulani katika tasnia hiyo ya mziki alijaribu kumtilia sumu ili kumzuia kuhubiri injili.
Ilagosa pia alikuwa mchungaji na mwanzilishi wa huduma ya kimataifa ya kinabii Nyimbo zake nyingine ni pamoja na: Amba, Kamera ya Yesu na Sema nami.
Ameacha mtoto mmoja tangu alipotengana na mkewe kitambo.