Walimu Waliozuliwa Kisii Waachiliwa

Walimu sita waliozuiliwa wa Shule ya Msingi ya Itumbe DOK kwa tuhuma za kusambaza video chafu wameachiliwa kwa bondi ya Shilingi 500,000 kila mmoja.
Walimu hao walikamatwa baada ya klipu kusambaa mitandoni ambapo walinaswa wakiwalazimisha wanafunzi wa darasa la pili kuiga kufanya ngono.
Jana Jumatatu jioni, walifikishwa katika Mahakama ya Sheria ya Ogembo mbele ya Hakimu Mkuu Calestous Sindani Nambafu ambapo walikanusha mashtaka ya kuwatesa watoto hao kwa ukatili, unyama, udhalilishaji na adhabu na kitendo kisichofaa.
Walimu hao walikuwa wametumia muda wa ziada kuhama kutoka mahakama moja hadi nyingine kufuatia mzozo kati ya upande wa mashtaka na utetezi kuhusu wapi walipaswa kupeleka maombi yao.
Mnamo Ijumaa wiki jana, Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Ogembo, Paul Biwott aliagiza walimu hao wazuiliwe katika Kituo cha Polisi cha Nyangusu hadi jana (Jumatatu), ili kuruhusu maafisa wa uchunguzi kuandaa mashtaka dhidi yao.
Hata hivyo, Jumatatu asubuhi, walimu hao waliwekwa kwenye gari la polisi kutoka kituo cha polisi cha Nyangusu na kupelekwa katika Mahakama ya Kisii, ambapo walifikishwa mbele ya Hakimu Catherine Ocharo.
Wakitaja hatua hiyo kuwa mbaya, mawakili wao wakiongozwa na Edward Begi, walihoji ni kwa nini wateja wao walikuwa wakiwasilishwa katika mahakama tofauti ilhali kesi hiyo ilikuwa chini ya mamlaka ya Mahakama ya Ogembo.
Upande wa mashtaka ulisema polisi wamekamilisha upelelezi na maombi mengine yamekataliwa.
Hata hivyo, upande wa mashtaka haukuwasilisha nyaraka zozote kuthibitisha ni kwa nini walichukuwa hatua hiyo.
Walimu hao walirudishwa Ogembo ambako walishtakiwa.
Huduma ya Walimu TSC imechukua nafasi za wale sita Everlyne Moraa Orina, Catherine Mokaya, William Isuka, Druscilla Moraa, Angellica Joseph na Gladys Kenyanya na kuwaandika walimu wengine.