Absalom ‘Matakwey’ Aachiliwa
Mwakilishi wadi wa Korogocho Absalom Odhiambo almaarufu ‘Mobimba’ ameachiliwa na maafisa wa polisi baada ya kuzuiliwa kwa kutamka maneno yaliyokisiwa kusababisha vurugu wakati wa mkutano wa kisiasa kule kamkunji Nairobi.
Haya yanajiri baada ya mahakama kukataa ombi la Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) iliyotaka mwakilishi wadi huyo wa Kaunti ya Nairobi azuiliwe zaidi.
Mobimba alifikishwa mahakamani kwa madai ya matamshi ya chuki aliyotoa wakati wa mkutano wa Azimio huko Kamukunji ulioelekezwa kwa chama tawala.
Kwa mujibu wa Hakimu Mkuu wa Milimani Gilbert Shikwe, maombi yaliyowasilishwa hayakutokana na masharti yoyote ya kisheria.
Kulingana na wakili wake Apollo Mboya, kesi hiyo imetupiliwa mbali kwa kuzingatia kifungu cha 96-A cha kanuni ya adhabu ambayo ilitangazwa kuwa kinyume na katiba katika kesi ya uchochezi ya 2015 iliyomhusisha aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama.
Kifungu cha 96(a) cha sheria ya kanuni ya adhabu kinasema kwamba mzigo wa uthibitisho ni juu ya mtu yeyote anayetamka, au kuchapisha maneno yoyote au kufanya kitendo chochote kinachohesabiwa kuleta kifo au jeraha la kimwili kwa mtu mwingine, tabaka, au jamii.
Mnamo 2015, Muthama alipinga uhalali wa kikatiba wa mashtaka ya uchochezi kama ilivyoainishwa katika kifungu cha Kanuni ya Adhabu ambapo majaji wa Mahakama ya Juu waliagiza Bunge lifutilie mbali sehemu hiyo.
Sehemu hiyo hata hivyo bado haijarekebishwa kwa hivyo kosa la matamshi ya chuki halitambuliwi kisheria.
Mnamo Jumatatu, Januari 30, maafisa wa idara ya upelelezi na makosa ya jinai DCI walimkamata mwakilishi huyo katika afisi za Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) ambako alikuwa ameitwa kutokana na matamshi yake ya uchochezi.
Baadaye aliripotiwa kutoweka na wakili wake Apollo Mboya ambaye alidai kuwa Mobimba hakuwa katika kituo chochote cha polisi walichokipekua.