Viongozi Wa Kanisa Wasimame Tisti kurejesha Amani Nchini
Wakati viongozi wa muungano wa kenya kwanza wakihudhuria ibada ya shukurani katika kuanti ya Narok kushukuru kwa kuchaguliwa na wa upinzani wakiendelea kuhoji kuwa waliibiwa kura, viongozi wa dini wametakiwa kusimama imara kurejesha umoja wa kitaifa.
Akiongoza mkutano wa maombi ya shukrani uliowaleta pamoja viongozi wa kisiasa, mawaziri, viongozi wa kidini na maafisa wakuu wanaohudumu katika kaunti ya Nakuru, Gavana Susan Kihika amewahimiza viongozi wa kidini kudhihirisha mchango wao kwa umma na kutoa mwongozo unaofaa.
Mchango wa kanisa kwenye siasa umesababisha mdahalo mkubwa nchini hasa baada ya kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja one Kenya, Raila Odinga, kumkosoa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana, Jackson Ole Sapit, kwa kuhusika kwenye siasa na kuegemea upande wa mpinzani wake, Rais William Ruto, wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.
Kwa upande wake, Askofu Sapit ametoa wito kwa wanasiasa kupunguza cheche zao na badala yake kuzingatia utangamano wa Wakenya na namna ya kuboresha hali ya uchumi wa Wakenya.
Mkuu huyo wa Kanisa la Anglikana nchini Kenya amekuwa akihimiza usawa baina ya viongozi walioko serikalini na wale walio kwenye upinzani.
Gavana Kihika, ambaye alifunguliwa kesi mahakamani alipoanza tu mchakato wa kuunda serikali yake baada ya kutwaa ushindi kwenye uchaguzi wa Agosti, amesema kesi za mara kwa mara mahakamani zinakwamisha utoaji wa huduma kwa umma.
Gavana huyo ametumia hafla hiyo kutangaza kuanzishwa kwa miradi mbalimbali, ikiwemo kufufuliwa kwa mradi wa Bwawa la Itare unaofanywa kwa ushirikiano na Italia.
Rais William Ruto anatarajiwa kuongoza mkutano wa maombi ya shukrani utakaofanyika mjini Nakuru tarehe 12 mwezi ujao.
Mkutano huo utawaleta pamoja viongozi na Wakenya wa tabaka mbalimbali kutoka kote nchini.
Mji wa Nakuru ni eneo muhimu kwa siasa za taifa kutokana na kwamba una wananchi wa makabila mbalimbali na pia mingi ya mikataba ya kisiasa iliyotengeneza serikali imefanyika huko.