Hatutishwi! Raila Asisitiza Mkutano Wa Jacaranda Utaendelea

Kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja One-Kenya Raila Odinga amesisitiza kuwa mkutano wa Jacaranda uliopangwa bado unaendelea.
Katika tweet Jumamosi, Waziri Mkuu huyo wa zamani amesema hatatishwa na mtu yeyote na kuwaambia wafuasi wake kwamba wanakutana katika viwanja vya Jacaranda siku ya Jumapili, kwa ajili ya mkutano huo uliopewa jina la “No Handshake”.
Hatutishwi wala hatutatishwa. Tukutane Jacaranda!— Raila Odinga (@RailaOdinga) Januari 28, 2023
Haya yanajiri baada ya Rais William Ruto mnamo Ijumaa kusema kuwa hataruhusu mikutano ya Azimio isumbue kuwasilisha kwa Wakenya.
Rais Ruto alisema kuwa viongozi wa Azimio wanawatumia Wakenya kwa kuwataka kuhudhuria mikutano ya hadhara huku watoto wao wakiwa Arusha na Ulaya.
Aidha Ruto alisema wanachofanya ni sehemu ya mchakato wa mchezo wao mrefu kusalia muhimu huku wakisubiri kujaribu bahati yao katika afisi kuu.
Raila alifanya mkutano Jumatatu huko Kamukunji ambapo alisema hamtambui Ruto kama rais wa jamuhuri ya kenya.