Makau mutua asema Azimio itaendelea kushinikiza ushindi wao

Prof Makau Mutua, msemaji wa kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga, ameeleza kuwa hawataacha azma yao ya “ushindi” katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, ambao wanadai ulivurugwa na kumpendelea Rais William Ruto.
Mutua ameshutumu sheria ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na baadhi ya vyama vya kimataifa ambavyo alikataa kufichua utambulisho wao kwenye mahojiano na runinga moja humu nchini.
Prof Mutua aliendelea kusema kuwa walijadili suala hilo kwa miezi kadhaa tangu Rais ruto aapishwe na waliona inafaa kuliwasilisha kwa Wakenya sasa.
Vile vile amewataka wafuasi wa muungano wa azimio la umoja one-kenya waliokubali serikali ya Kenya kwanza kupinga utawala wa chama cha UDA, anachodai kuwa kilinyakua mamlaka kwa njia isiyo halali.
Mnamo Agosti 15, 2022, Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alimtangaza Ruto kuwa rais mteule baada ya kupata kura 7,176,141, sawa na asilimia 50.49 ya kura zote zilizopigwa, huku Odinga akipata kura 6,942,930, ikiwa ni asilimia 48 ya kura zilizopigwa.
Kiongozi wa chama cha Narc-Kenya Martha Karua vile vile ametaka sava zote za IEBC kufunguliwa kwa umma ili kuchunguza ukweli wa kujumlisha kura za urais.