Pesa Za NG-CDF Zaanza Kutumwa Katika Kaunti Mbalimbali
Mzozo unaohusu utolewaji wa fedha za maendeleo ya maeneobunge NG-CDF kati ya Hazina na Wabunge , umetatuliwa Jana kufuatia kikao cha faragha kilichoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula.
Wabunge hao, wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati ya NG-CDF Musa Sirma, walisema serikali imetoa shilingi bilioni .4 na itatoa shilingi bilioni .2 zaidi leo hii Alhamisi.
Wabunge hao sasa wanatazamiwa kurefusha warsha yao ya kujitambulisha hadi Jumamosi ili kufidia siku zilizopotea kutokana na mvutano huo kule Mombasa.
Itakumbukwa kwamba wabunge hao walikuwa wamesusia mkutano huo wa kuwatambulisha katika bunge hadi serikali itekeleze majukumu yake kwa kutuma fedha hizo katika serikali za kaunti, kwani wazazi waliokuwa wakitafuta basari walikuwa wamepanga foleni ndefu katika afisi zao bila mafanikio, huku shule zikiendelea kuwatuma nyumbani wanafunzi wasio na karo.
Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, kwa upande wake, amesema Hazina ya Kitaifa ililazimika kutoa fedha kwa ajili ya shule za msingi na sekondari za umma jambo ambalo pia lilisababisha kuchelewa.
Kufikia mwisho wa juma lijalo, wabunge hao wanatarajia kuwa wamepokea angalau shilingi milioni .50 zinazogharamiwa kwa ajili ya basari na gharama nyinginezo za usimamizi.