Maafisa Wanne Eldoret Watuhumiwa Kwa Mauaji

Mahakama ya Eldoret imeamuru kukamatwa kwa watu wanne akiwemo Chifu wa lokesheni ya Kaptebee, kiongozi mmoja wa eneo hilo na wazee wawili wa Nyumba Kumi kutokana na kifo cha kutatanisha cha mwanamke mmoja katika eneo hilo.
Hakimu Mkuu Mkaazi wa Eldoret Barnabas Kiptoo ameagiza kukamatwa kwa wanne hao ili wafunguliwe mashtaka kuhusiana na kifo cha Mercy Cheptoo mwenye umri wa miaka 23 anayesemekana kufanya biashara ya pombe haramu.
Kufuatia uchunguzi ulioanza Machi 2020, mahakama iligundua kuwa cheptoo alifariki akiwa mikononi mwa wanne hao wakati wa oparesheni dhidi ya pombe haramu katika kijiji cha Kaptebee huko Turbo, Kaunti ya Uasin Gishu.
Wakati wa msako huo, mwanamke huyo ambaye ni mama ya watoto wawili, anasemekana kujaribu kutoroka alipokuwa akikimbia kuelekea mtoni huku akiomba huruma kutoka kwa wanne hao.
Watuhumiwa hao waliieleza mahakama kuwa marehemu alifariki dunia baada ya kutumbukia mtoni, lakini mahakama ilibaini kuwa marehemu pia alikuwa na majeraha kichwani yaliyotokana na kupigwa kwa kifaa butu kwa mujibu wa uchunguzi wa mwili wa marehemu mama huyo.
Mahakama iliamuru kukamatwa kwa wanne hao ikiwa hawataripoti katika Kituo cha Polisi cha Eldoret Magharibi ndani ya siku saba ili wafunguliwe mashtaka.