Mudavadi Apongeza Uwekaji Huduma Katika Mfumo Wa Kidijitali
Waziri Mkuu Musalia Mudavadi amepongeza uwekaji wa huduma za serikali katika mfumo wa kidijitali akisema utasaidia kukabiliana na ufisadi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kurejea nyumbani na kutoa shukrani kwa mbunge wa Tongaren John Chikati, Mudavadi amesema enzi za maafisa wa serikali kuomba hongo zimepitwa na wakati.
Mudavadi ameendelea kusema kuwa serikali itatoa kila msaada unaohitajika kwa Waziri wa Afya Nakhumicha katika vita dhidi ya ufisadi katika wizara yake ambapo maafisa wa KEMSA wamekumbwa na kashfa za mabilioni ya pesa.
Matamshi ya Mudavadi yanakuja baada ya angalau huduma 5000 za kidijitali kutolewa Ijumaa kwenye mtandao wa e-Citizen ambao ni lango la serikali kwa huduma za mtandaoni.
Kwa kuimarika kwa muunganisho wa intaneti katika maeneo ya mijini na vijijini na idadi ya watu walio na ujuzi wa teknolojia, programu mpya ya simu ya Gava Mkononi iliyozinduliwa na serikali inakuja kwa manufaa.
Hii pia ni kwa kuzingatia ukweli kwamba watumiaji wengi wana simu mahiri hivyo kurahisisha ufikiaji wa huduma.
GAVA EXPRESS
Huduma mashinani zimeboreshwa kwa kuanzishwa kwa Gava Express ambayo ina muundo wa Huduma Centers.
Tofauti na Huduma Centers ambazo kimsingi ziko katika makao makuu ya kaunti, Gava Express itatoa huduma mashinani.
Gava Express itaendeshwa kwa ushirikiano na sekta binafsi na inalenga uanzishwaji wa maduka zaidi ya 300,000.
Hatua hiyo muhimu ni sehemu ya hatua kubwa ambayo Kenya imepiga katika upatikanaji wa kidijitali tangu utawala wa Kenya Kwanza kuchukua mamlaka mwaka jana.
Huduma 10 maarufu zaidi kwenye jukwaa la e-Citizen ni:
NTSA – Leseni ya Muda ya Kuendesha gari
Huduma za Usajili wa Biashara
Kibali cha Polisi / Cheti cha Maadili Mema
Huduma za Usajili wa Kiraia – Ndoa
Usajili wa Awali wa Raia wa Kigeni
Kurugenzi ya Huduma za Uhamiaji
Mamlaka ya Bandari ya Kenya
Mamlaka ya Mapato ya Kenya
HELB
MSMEs (Hustler Fund)