Jubilee Yapuuza Kuondoka Azimio
Kambi inayomuunga mkono Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta imepuuzilia mbali notisi inayotaka chama cha Jubilee kuondoka Azimio.
Mrengo huo unaoongozwa na Jeremiah Kioni, katibu mkuu wa chama aliyefukuzwa umewataka wanaotaka kuondoka kufanya hivyo ”kimya”.
”Chama cha Jubilee kiko Azimio kubaki. Tunawaomba wale ambao wanahisi kuchoshwa na sababu hii, waondoke kimya kimya hadi kwenye karamu ambapo watakuwa na starehe zaidi,” timu ya Kioni ilitweet Jumanne.
Hapo awali, mrengo wa chama cha Jubilee unaoongozwa na kaimu Katibu Mkuu Kanini Kega ulikuwa umeandikia Muungano wa Azimio la Umoja kuarifu uongozi kuhusu notisi ya kujiondoa.
Katika taarifa yake, Kega alisema uamuzi huo umefikiwa kufuatia kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichoketi Juni 6.
Lakini timu ya Kioni ilitaja notisi hiyo kuwa ghushi.
Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu hivi majuzi aliidhinisha mrengo wa Kega kuwa viongozi wa dhati wa chama cha Jubilee.
Hata hivyo, timu ya Kioni ilihamia mahakama hiyo kupinga uamuzi huo.