Waziri Kindiki Awaonya Wabunge Wa Azimio Dhidi Ya Maandamano

Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa Kithure Kindiki amewataka wabunge washirika wa Azimio la Umoja One-Kenya wajizuie kufanya maandamano kupinga Mswada wa Fedha wa 2023.
Akizungumza jana Jumapili wakati wa ibada katika kanisa la Tharaka Nithi, waziri huyo amewataka wabunge hao kujadili maoni yao yanayopingana kuhusu mswada huo bungeni na kuacha maandamano, akisema wanalenga kuharibu mali na kutatiza shughuli za biashara jijini Nairobi.
Kauli za waziri wa mambo ya ndani zinajiri baada ya viongozi wa Azimio la Umoja kutishia kurejelea maandamano iwapo Mswada wa Fedha utapitishwa na Bunge.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amepuuzilia mbali mapendekezo ya mswada huo akisema yataathiri uchumi wa Kenya na kuongeza kuwa itakuwa mzigo mkubwa kwa walipa ushuru ambao tayari wameelemewa.
Aidha, Waziri Mkuu ametoa onyo kwa viongozi ambao watachochea umma kuharibu mali za watu wakati wa maandamano akisema kuwa serikali haitaruhusu maandamano kama hayo.
Hata hivyo amewaruhusu watu kushiriki maandamano ya amani akisisitiza kuwa ni haki iliyoainishwa katika katiba ya Kenya.
Waziri huyo ameendelea kugusia visa vya ujambazi huko Tharaka Nithi akisema kuwa serikali itapeleka Kitengo cha Kupambana na Wizi ndani ya mwezi mmoja katika kaunti hiyo kama hatua ya kukabiliana na tishio la wizi wa mifugo na ugaidi.