Home » KeNHA Yaweka Alama Za Kudhibiti Magari Kwenye Barabara Kuu Ya Nairobi-Nakuru

KeNHA Yaweka Alama Za Kudhibiti Magari Kwenye Barabara Kuu Ya Nairobi-Nakuru

Watumiaji wa barabara kuu ya Nairobi-Nakuru yenye shughuli nyingi wana sababu ya kutabasamu baada ya serikali kuingilia kati na kuashiria maeneo hatari yaani (BLACK SPOTS) kwa kuweka alama za barabarani kushughulikia visa vya ajali mbaya.

 

Chini ya zoezi la Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu (KeNHA), alama za barabarani za hivi punde zaidi zimewekwa karibu na Naivasha ambapo zaidi ya watu 30 wamefariki tangu mwaka uanze.

 

Zoezi hilo linajiri wiki chache baada ya Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) kuonya kuhusu ongezeko la ajali mbaya katika barabara kuu.

 

Kufuatia hatua hiyo, wakaazi na madereva wanaotumia barabara hiyo wamekaribisha mpango huo wakibainisha kuwa tayari idadi ya ajali imepungua katika muda wa wiki kadhaa zilizopita.

 

Kulingana na Dan Wainaina mkaazi wa Kinungi huko Naivasha, zoezi la KeNHA lilifanyika wakati mwafaka na limesaidia kukabiliana na idadi ya ajali.

 

Ametoa wito wa vikwazo zaidi vya mwendo kasi kati ya kituo cha biashara na mji wa Naivasha kama njia mojawapo ya kupunguza mwendo kasi miongoni mwa madereva.

 

Haya yameungwa mkono na mkazi mwingine John Karanja ambaye ametaja alama za barabarani kama hatua nzuri kwa waendeshaji magari na abiria wa kawaida.

 

Hata hivyo, ameelezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa visa vya uharibifu vinavyolenga ishara za barabara na kuongeza kuwa hii itaondoa maeneo halisi yaliyowekwa alama.

 

Mfanyabiashara, Silas Maasai naye ametoa wito wa kuwepo kwa alama zaidi za barabarani kando ya barabara kuu yenye shughuli nyingi na hasa sehemu hatari zilizokuwa zimejaa mashimo hivyo kuendekeza ajali kutokea.

 

Akizungumza wiki mbili zilizopita, Mkurugenzi Mkuu wa NTSA George Njau, alisema wanashirikiana na KeNHA kuongeza alama za barabarani kando ya barabara hiyo na kurekebisha mashimo.

 

Njau alisema kuwa mamlaka hiyo inaweka mifumo ya usimamizi na usalama wa barabara inayolenga magari ya umma kama sehemu ya kupunguza ajali za barabarani.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!