Uhasama Baina Ya Ruto, Raila Waonekana Bungeni

Mvutano kati ya washirika wa Rais William Ruto na wale wa kinara wa Upinzani Raila Odinga unatishia kuzorotesha hali ya makubaliano kuhusu mjadala mswaada wa fedha 2023 Jumanne wiki ijayo vile vile mazangumzo ya pande mbili Bipartisan.
Aidha Shughuli muhimu zilizopangwa katika Bunge na juhudi za kufufua mazungumzo ya pande mbili ziko katika hatari ya kutupwa nje.
Dalili za kutatanisha zilianza Alhamisi baada ya wabunge wa Azimio kuzozana na Spika Moses Wetangula kwa kukosa kumwondoa Mbunge Mteule Sabina Chege kama naibu kinara wa wachache.
Kikao cha Bunge kilimalizika kwa sintofahamu iliyoshuhudia mkono wa Sabina ukiwa umejeruhiwa katika vurugu hizo.
Wetangula katika uamuzi wake alisema mikono yake ilikuwa imefungwa kufuatia agizo la mahakama lililozuia mabadiliko hayo.
Upinzani unamtaka Sabina aondoke kwenye wadhifa wake mkubwa kuhusu ushirikiano wake na muungano wa Ruto wa Kenya Kwanza.
Machafuko hayo yalisababisha wabunge saba kusimamishwa kuhudhuria vikao kwa siku tofauti kufuatia mzozo huo.
Millie Odhiambo (Suba Kaskazini), Roza Buyu (Kisumu Magharibi), TJ Kajwang (Ruaraka) na Chege walisimamishwa kuhudhuria vikao kwa wiki mbili.
Mwenzao wa Malindi Amina Mnyazi na Catherine Omanyo wa Busia walifungiwa kwa siku tano.
Mwakilishi wa Wanawake wa Machakos Joyce Kamene alisimamishwa kuhudhuria vikao viwili.
Hali hiyo imefichua mvutano unaoongezeka kati ya kambi za Raila na Ruto kabla ya mjadala kuhusu Mswada wa Fedha siku ya Jumanne.
Raila ametangaza kuwa ana mpango wa kukabiliana na mapendekezo ya sheria ya ushuru, ndani ya Bunge na nje, na hivyo kuweka mazingira ya mzozo mkubwa.
Kiongozi huyo wa ODM amemtaka Ruto kuondoa Mswada wa Fedha na kuzingatia kupunguza gharama ya maisha kama kipaumbele.
Vile vile Kiongozi huyo wa upinzani anataka timu ya Kenya Kwanza kupunguza bajeti na kuishi kulingana na uwezo wake.
Msimamo huo huenda ukapingwa na wabunge wa Kenya Kwanza ambao wakuu wao wameagizwa vikali kupitisha mswada huo bila marekebisho yoyote.
Rais Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua wote wameonya wabunge wao kuhusu madhara ambayo hayajabainishwa iwapo watakaidi mwito wao wa kuunga mkono Mswada wa ushuru.
Akiwa katika Kongamano la Kahawa huko Meru siku ya Ijumaa, naibu rais alidokeza timu ya azimio ilikata tamaa ‘ambayo imeanza kupigana badala ya kujihusisha na mjadala wa maana’.
Upande wa wabunge wa Raila wanashikilia kuwa tatizo hilo linatokana na hofu kwamba Spika Wetangula anacheza kama Mtendaji Mkuu.
Hisia za jumla katika kambi ya Raila ni kwamba timu ya Ruto inajinufaisha na idadi yake ya wabunge wengi kutunga sheria kwa kuikatisha tamaa Azimio.
Hata hivyo, kuna manung’uniko ya wabunge wengi wao kutoka Azimio na sehemu ya Kenya Kwanza, kuhusu kucheleweshwa kwa pesa za CDF.
Kadhalika Wametishia kutatiza hotuba ya bajeti ya Waziri wa Hazina Njuguna Ndung’u Alhamisi ijayo ikiwa CDF haitatumwa kwenye akaunti za maeneo bunge.