Noordin Haji: Miaka Yangu 6 Kama DPP Imekumbwa na Vita Vikali

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji amedokeza kuwa miaka yake 6 ya uongozi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) haijawa rahisi kutkeleza sheria katika nafasi yake.
Akizungumza wakati wa mkutano wa mashauriano ulioongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei ,DPP Haji amesema kuwa muda wake umekumbwa na mizozo na taasisi nyingine ambazo anasema zilikuwa zikijaribu kupindua utawala wa sheria kwa manufaa yao.
Akikemea kukithiri kwa visa vya ufisadi katika taasisi za serikali, Haji alibainisha kuwa ni wakati mwafaka wa kutii sheria na kutumikia kwa uadilifu.
Wakati uo huo, Haji anatarajiwa kufika mbele ya Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Idara ya Ujasusi na Mahusiano ya Kigeni ya Bunge la Kitaifa ili kuhakiki uteuzi wake wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS).
Haji, afisa mkuu wa zamani katika shirika la kijasusi, ambapo alihudumu kama naibu mkurugenzi wa kitengo cha uhalifu uliopangwa, atachukua nafasi ya Meja-Jenerali Mstaafu Philip Kameru ikiwa ataidhinishwa na Bunge.