Richard Onyonka: Kuchagua Ruto Ni Kifumbua Macho Kwa Wakenya
Seneta wa Kisii Richard Onyonka ameelezea utawala wa Rais William Ruto kama kifumbua macho kwa Wakenya.
Akitoa mfano wa tozo mbalimbali zilizopendekezwa katika Mswada tata wa Fedha wa 2023, Onyonka amesema hii leo Jumanne licha ya kuwepo kwa msukosuko huo, kuna uwezekano mkubwa kwamba mswada huo utapitishwa bungeni kutokana na amri za muungano wa Ruto wa Kenya Kwanza katika Bunge hilo.
Seneta huyo, ambaye amekuwa akizungumza kwenye runinga humu nchini, amebainisha kuwa mswada huo utawafanya Wakenya kuelewa athari za ajenda ya Kenya Kwanza na kutoa mafunzo kwa uchaguzi zijazo.
Kulingana na seneta huyo, Wakenya katika siku zijazo watakuwa wakiwatathmini wagombeaji urais kabla ya kupiga kura ili kuchunguza ajenda zao na jinsi zinavyoathiri gharama ya maisha wakati wanapewa mamlaka.