Migori: Watu 4 Wauawa Wakijaribu Kuiba Bunduki Katika Kituo Cha polisi
Watu wanne wameuawa kwa kupigwa risasi katika Kaunti ya Migori wakati wa uvamizi mkali wa Kituo cha Polisi cha Isebania na majambazi waliokuwa wamejihami.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi kuhusu tukio hilo la saa 6:30 jioni, kundi la watu waliokuwa wakiendesha gari kwa kasi lilifika kituo cha polisi wakisindikiza mwili wa mtu mmoja uliokuwa ukihamishwa na polisi kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya St.Akidiva Mindira Mabera.
Baada ya kufika kituoni hapo, majambazi hao wanadaiwa kutumia mapanga na mawe ambayo yalikuwa yamefichwa kwenye gari hilo na kwenda mbele kuvamia kituo hicho.
“Walivunja madirisha ya ghala la silaha za kituo, ofisi ya OCS na ofisi zingine kwa mawe. Walianza kuharibu milango ya seli wakitaka wafungwa wote walioko kizuizini waachiliwe,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Maafisa wa polisi kisha walilazimika kutumia bunduki baada ya kundi hilo kuvamia ofisi ya ripoti, na ghala la silaha na sasa walikuwa wakielekea kwenye seli ili kuwaachilia wafungwa waliokuwa wamefungwa.
Kulingana na polisi huko Migori, shambulio hilo lilipangwa na washukiwa watatu ambao wamehusishwa na kisa hicho.
Waliotajwa kuwa ni Peter Hamisi Chacha, John Musa na Nsato almaarufu Manywele, ambaye anaripotiwa kuendesha gari hilo lililojaa mawe.
Polisi walilazimika kutumia vitoa machozi kuwatawanya waasi hao kutoka kituo cha polisi.
Afisa mmoja wa polisi aliyekuwa akilinda ghala la silaha alipata majeraha kwenye jicho la kulia na majeraha mengine ya mwili baada ya kupigwa na umati huo.
Miili ya washukiwa wanne waliopigwa risasi katika kituo hicho ilihamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya St. Akidiva Mindira Mabera.