JSC Yafichua Ulaghai Mpya Unaolenga Wakenya

Idara ya Mahakama, kupitia notisi rasmi imeonya Wakenya kuhusu kashfa mpya inayolenga raia wasio na ajira.
Katika notisi iliyotiwa saini na Kurugenzi ya Masuala ya Umma na Mawasiliano ya Biashara katika Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), Wakenya wengi waliripotiwa kupoteza pesa zao walizopata kwa bidii yao baada ya kudanganywa kutuma ili kutayarishiwa stakabadhi za kusafiri.
Aidha idara hiyo imewataka Wakenya ambao walikuwa wametuma maombi ya kazi mbalimbali katika Idara ya Mahakama kusubiri mawasiliano kutoka kwa njia rasmi.
Visa vya kundi la watu wanaotumia fursa ya Wakenya wanaotafuta kazi vimeongezeka tangu mwanzo wa 2023.
Mnamo Alhamisi, Mei 18, Waziri wa Masuala ya Kigeni Alfred Mutua alionya Wakenya dhidi ya kulaghaiwa kupitia kazi ghushi zinazotolewa nchini Kanada.
Siku iyo hiyo, serikali ya Ujerumani ilijutia ongezeko la walaghai mtandaoni wakiwaahidi Wakenya kazi zenye ujuzi katika nchi hiyo ya Ulaya.
Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) inawataka waathiriwa kuripoti udanganyifu wa kazi kupitia simu kupitia +254 020 3343312, nambari ya simu 020 7202000 au nambari ya bure 0800 722.