Mahakama Yairuhusu Serikali Kuchukua Ksh.102M Za Mwanafunzi Mkenya
Mahakama Kuu imeiruhusu serikali kuchukua zawadi ya pesa ya Ksh102 milioni iliyotumwa kwa mwanafunzi wa umri wa miaka 23 Felista Nyamathira Njoroge na mpenzi wake bilionea wa ng’ambo (mbelegiji).
Katika hukumu iliyotolewa na jaji Esther Maina hii leo Alhamisi, Mei 25, 2023, serikali ya Kenya imeruhusiwa kuhifadhi pesa zilizokuwa katika akaunti mbili za Benki ya Co-operative ya Nyamathira baada ya kuthibitisha zawadi hiyo iliyotokana na mtandao wa ufujaji wa pesa.
Jaji huyo aliamuru kunyang’anywa kwa fedha hizo kwa vile chanzo cha pesa hizo hakikuwa kimeelezwa na kufichuliwa na bilionea Marc De Mesel, mhusika maarufu wa YouTube wa Ubelgiji.
Katika uamuzi wa kihistoria, Jaji Maina amesema mfadhili huyo alipewa fursa ya kueleza jinsi anavyopata pesa zake ambazo huwapa wanawake vijana kote ulimwenguni apendavyo lakini alishindwa kufanya hivyo.
Jaji Maina amesema kwa kukosekana kwa maelezo, serikali inanufaika na pesa zilizoingizwa kwa siri nchini kutoka kwa mtu wa ng’ambo ambaye kulingana nao hajajulikana vyema.
Huku akiruhusu ombi la shirika la Urejeshaji Mali (A.R.A) kutaka fedha hizo zitangazwe kama mapato ya uhalifu, Maina amesema kuwa ushahidi uliotolewa mahakamani na serikali na wapenzi hao wawili ulibaini kuwa kulikuwa na utakatishaji fedha.
“Nilichambua na kupitia ushahidi uliotolewa na mpenziwe na haukuonyesha chanzo cha pesa ambazo zilitumwa kwa rafiki wa kike wa Kenya,” akaamua Jaji Maina.
Vile vile ameongeza kuwa kwa kukosekana kwa ufichuzi wa chanzo cha fedha, hitimisho linalowezekana ni kwamba chanzo cha pesa ni kinyume cha sheria.
Kutokana na hali hiyo, alisema, mahakama haina njia mbadala zaidi ya kuamuru fedha zilizo katika akaunti mbili za benki zichukuliwe kwa serikali.
Nyamathira aligonga vichwa vya habari mnamo 2021 alipotangaza hadharani kwamba makachero kutoka idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI walinasa zawadi ya pesa aliyotumiwa na mpenzi wake wa Ubelgiji.
Mwanamke huyo alilalamikia kudhulumiwa na shirika la uhalifu la serikali kwa kumnyima Ksh102 milioni alizotumwa kwa matumizi yake ya kibinafsi.
Ushahidi uliotolewa mahakamani ulionyesha kuwa mamilioni hayo yaliwekwa kwenye akaunti katika Benki ya Co-operative katika miamala minne kati ya Agosti 4 na Agosti 6, 2021, jambo lililozua shaka kutoka kwa mamlaka.
Tajiri huyo pia aliangaziwa baada yake pia kuwatumia Ksh257 milioni wanawake wengine watatu wa Kenya ambao ni Tabby Wambuku Kago (Ksh108 milioni), Jane Wangui Kago (Ksh49 milioni), na Serah Wambui (Ksh100 milioni).
Mbelgiji huyo alituma $229,980 mnamo Agosti 4, ikifuatiwa na $231,980 siku iliyofuata.
Mnamo Agosti 6, Mesel alituma pesa hizo mara mbili, $224,980 na $227,980 kwenye akaunti ya benki ya Nyamathira.
Pia aliambia mahakama kuwa alimpa mwanamke huyo pesa hizo kama zawadi kutokana na mapenzi yao.
ARA ilidai kuwa raia huyo wa Ubelgiji na Nyamathira wanaweza kuhusika katika mpango wa kimataifa wa utakatishaji fedha.
Mwezi mmoja baada ya ARA kuwasilisha shtaka hilo, utambulisho halisi wa mwanamke aliyepelekewa pesa hizo ulitiliwa shaka Januari 26, 2022, baada ya vikundi viwili vya mawakili kuzozana mahakamani na kuzungumzia kuhusu watu tofauti.
Jaji katika hukumu yake amekataa kuangazia suala la uwakilishi wa kisheria wa Nyamathira.