Vyombo Vya Habari Vyaombwa Kuwa Macho Kuhusu Shughuli Za Kamari
Baraza la Vyombo vya Habari nchini (MCK) limewataka wanahabari pamoja na vyombo vya habari kuwa macho kuhusu uendelezaji wa shughuli za michezo ya bahati nasibu kwenye majukwaa ya vyombo vya habari.
Katika taarifa, Mkurugenzi Mtendaji wa MCK David Omwoyo, amesema kuwa baraza hilo limebaini kuwa wasiwasi inaendelea kuongezeka kwa matangazo na ukuzaji wa shughuli za michezo ya kubahatisha, ambazo baadhi yake hazijaidhinishwa na Bodi ya Kudhibiti na Kutoa Leseni za Kamari (B.C.L.B).
Omwoyo amewashauri waandishi wa habari, watendaji wa vyombo vya habari, na makampuni mbalimbali kuhakikisha kwamba matangazo ya mashirika ya michezo ya bahati nasibu yaliyopewa leseni na B.C.L.B pekee ndiyo yanayopeperushwa kwenye majukwaa yao.
Wakati huo huo Omwoyo amewataka wanahabari kuheshimu Kanuni za Maadili ya Uandishi wa Habari nchini Kenya ambayo inawataka wanahabari, watendaji wa vyombo vya habari, na makampuni ya biashara kuandika habari za haki, sahihi na zisizo na upendeleo kuhusu masuala ya maslahi ya umma.