Watu Wanne Wafariki Katika Ajali Ya Basi Kajiado
Watu wanne wamefariki katika ajali mbaya ya barabarani eneo la Isinya, Kaunti ya Kajiado baada ya basi la abiria 40 lililokuwa likisafirisha wafanyikazi wa kampuni ya maua likielekea upande wa Kiserian kubingiria mara kadhaa.
Katika ajali hiyo ya saa 7:30 asubuhi, basi hilo ambalo kwa mujibu wa walioshuhudia wa gari hilo lilikuwa katika mwendo kasi na kushindwa kumudu udhibiti na kubingiria mara kadhaa huku watu wanne waliokuwa ndani ya gari hilo wakiripotiwa kufariki papo hapo huku wengine kadhaa wakijeruhiwa vibaya.
Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Isinya Patrick Manyasi, ametaja tukio hilo kuwa la kusikitisha akisema abiria wengi walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Kajiado wakiwa katika hali mbaya.
Amewataka madereva wote wa barabara kuwa waangalifu na kuepuka matukio ya mwendo kasi ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
Wenyeji waliokuwa karibu na eneo la ajali wamekashifu ongezeko la ajali katika eneo hilo wakiwataka viongozi kuweka alama na matuta katika eneo hilo.
Wanasema kona hiyo kali ni hatari kwa ajali na ni hatari kwa madereva hasa watumiaji wa mara ya kwanza wa barabara hiyo.
Basi hilo husafirisha wafanyikazi kwenda na kutoka shamba la maua la Ngong Veg na kwa kawaida hufanya safari mbili asubuhi na jioni.
Wakati ajali hiyo inatokea, basi hilo lilikuwa likisafiri kwa safari ya pili.