Home » Gachagua Adai Suala La Shakahola Ni Dogo

Naibu Rais Rigathi Gachagua sasa anasema serikali ina nia ya kuondoa tu vikundi vya kidini potovu na haitadhuru kwa vyovyote au kuingilia utendakazi wa makanisa katika uondoaji wa madhehebu ya kidini unaoendelea nchini.

 

Gachagua ambaye ametetea kanisa kama nguzo muhimu katika jamii amesisitiza kuwa matukio katika msitu wa Shakahola kaunti ya Kilifi ni suala dogo ambalo halifai kuchukuliwa kama shughuli inayofanyika katika taasisi zote za kidini.

 

Gachagua amebainisha kuwa katiba chini ya Ibara ya 32 inahakikisha uhuru wa kidini ikiwa ni pamoja na uhuru wa kufuata dini au imani yoyote na kwa hivyo, serikali haiko katika dhamira ya kuingilia uhuru huo.

 

Akiongea katika kanisa la Full Gospel Church eneo la Matangi huko Juja wakati wa misa ya kumuombea marehemu John Ndung’u, babake mbunge wa Juja George Koimburi, Naibu rais hata hivyo, amesisitiza kwamba viongozi wahuni ni lazima wataondolewa kutoka kwa umma ili kuwalinda Wakenya wanyonge.

 

Naibu rais ametoa kauli hiyo wakati Wakenya na viongozi wakishikilia miito ya udhibiti wa makanisa baada ya kubainika kuwa baadhi yao wamekuwa wakijihusisha na vitendo visivyokubalika.

 

Ametoa kauli hiyo siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki kutaka hatua kali zaidi zichukuliwe ili kudhibiti shughuli za kidini nchini ikiwa ni pamoja na kujidhibiti kwa mashirika hayo.

 

Haya yanajiri wakati mchakato wa kuunda sheria ya kudhibiti shughuli za kidini nchini ukianza baada ya Seneti mwezi uliopita kuunda kamati na kupendekeza sheria zinazolenga kuleta haki katika taasisi za kidini kuundwa.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!