COTU Yamtetea Rais Ruto Kuhusu Pendekezo La Ushuru
Muungano Mkuu wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) umekosoa vyama vingine ambavyo vinapinga pendekezo la ushuru wa nyumba lililotolewa na rais William Ruto.
Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli katika taarifa amesema kuwa amezungumza na Rais William Ruto na viongozi wote wa muungano huo kuhusu suala hilo na kukubaliana na hata kuona manufaa kuhusiana na jambo hilo.
Atwoli ametaja Kifungu cha 43 (b) cha Katiba, ambacho kinasema kwamba kila Mkenya ana haki ya viwango vinavyofaa vya hali ya usafi pamoja na makazi yanayofikika na ya kutosha.
Itakumbukwa kwamba Rais Ruto alisema serikali itaimarisha Hazina ya Makazi ili kuwasaidia Wakenya wengi zaidi kununua nyumba za bei nafuu.
Rais alisema Wakenya sasa watakuwa wakichangia asilimia 3 ya mapato yao na kuanza safari yao ya kumiliki nyumba.
Aliongeza kuwa mpango wa serikali wa kuongeza michango ya wanachama kwenye Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) umesaidia nchi kuongeza akiba yake ambapo pia imesaidia nchi kusimamia deni lake la nje kwa kutokopa zaidi.