Lionel Messi Asimamishwa Na PSG Kwa Wiki Mbili
Nahodha wa Argentina Lionel Messi amesimamishwa na klabu ya Paris St-Germain kwa muda wa wiki mbili baada ya kusafiri kwenda Saudi Arabia bila kibali cha klabu hiyo wiki hii.
Safari hiyo ilifuatia klabu hiyo ya Ufaransa kushindwa nyumbani na Lorient siku ya Jumapili, ambapo Messi alicheza dakika zote 90.
Messi hatafanya mazoezi wala kuichezea PSG katika kipindi cha kusimamishwa kwake.
Inafahamika kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 aliomba ruhusa ya kufanya safari hiyo ila wakala wamekana madai hayo.
Messi ambaye pia amepigwa faini na klabu hiyo ana jukumu la kuwa balozi wa utalii nchini Saudi Arabia.
Mkataba wa mshindi huyo wa Kombe la Dunia wa miaka miwili na PSG unamalizika msimu huu wa joto.
Makamu wa rais wa Barcelona Rafael Yuste alidai mwezi Machi kwamba klabu hiyo ya Uhispania ilikuwa inawasiliana na Messi kuhusu kurejea Nou Camp.
Messi amefunga mabao 31 na kutoa asisti 34 katika michezo 71 katika mashindano yote akiwa na PSG, na alishinda taji la Ligue 1 msimu uliopita.
Anatazamiwa kukosa mechi dhidi ya Troyes na Ajaccio akiwa PSG, akiwa mbele kwa pointi tano huku zikiwa zimesalia mechi tano, akitarajia kutwaa taji la tisa la ligi katika misimu 11.