Mwanafunzi Wa Chuo Kikuu Cha Maasai Mara Auawa
Polisi katika Kaunti ya Narok wanachunguza mauaji ya mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa kike wa Chuo Kikuu cha Maasai Mara ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa kwenye kichaka mita chache kutoka chuo hicho kikuu.
Marehemu aliyetambuliwa kama Adah Nyambura Ameru, mwenye umri wa miaka 20, alikuwa ameripotiwa kutoweka siku ya Jumapili na mpenziwe mwenye umri wa miaka 23, Brian Kimutai.
Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Narok, John Kizito, marehemu alitoweka Jumamosi usiku akiwa kwenye klabu ya usiku, kama ilivyoripotiwa na mpenziwe.
Baadaye mwili huo uligunduliwa katika eneo la Macedonia na wananchi ambao waliripoti tukio hilo kwa polisi.
Kamanda huyo wa polisi alisema mwili huo ulikuwa nusu uchi ukiwa na michubuko midogo usoni, na inashukiwa kuwa marehemu alibakwa kabla ya kuuawa.
Kulingana na video ambayo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii, mwanafunzi huyo alionekana akiwa katika hali nzuri, akicheza dansi kwenye klabu hiyo ya usiku, saa chache kabla ya kutoweka.
Mwili wake ulipelekwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Narok kwa uhifadhi ukisubiri uchunguzi wa maiti.
Aidha Wanafunzi wa vyuo vikuu kuuawa katika mazingira yasiyoeleweka kumeongezeka nchini.
Mwezi uliopita, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta June Jerop mwenye umri wa miaka 36 alidaiwa kuuawa na mpenzi wake katika mazingira yasiyoeleweka.
Mwezi uo huo, mwili wa Ann Wangari, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Bomet mwenye umri wa miaka 22 ulipatikana kutoka River Nyanogres wiki moja baada ya kutoweka.
Mnamo Januari mwili wa Phyllis Jepleting, ambaye wakati huo alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Karatina ulipatikana ndani ya nyumba ya mpenzi wake huko Nakuru.
Kizito alitoa wito kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kuzingatia masomo yao akisema michango yao inahitajika sana katika kuendeleza taifa.