Home » Polisi: Maandamano Ya Azimio Ni Haramu

Polisi wamemnyima kinara wa Upinzani Raila Odinga idhini ya muungano wa Azimio kufanya maandamano dhidi ya serikali jijini Nairobi kuanzia Jumanne wiki ijayo.

 

Katika taarifa yake Jumapili asubuhi, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nairobi Adamson Bungei alisema kuwa maandamano hayo sasa yameharamishwa kwa sababu hawakuonyesha nia njema katika maandamano ya awali.

 

Aidha, alisema maandamano hayo yalisababisha uharibifu wa mali, mashambulizi dhidi ya wananchi kwa jumla, kuiba, kupora na kuuawa Wakenya kadhaa.

 

Kulingana na Kamanda huyo maandamano kama hayo yatadhibitiwa na maafisa wa kutekeleza sheria ili kuhakikisha usalama wa Wakenya.

 

Kauli ya afisa huyo wa polisi inajiri siku moja baada ya Rais William Ruto kuapa kutumia uwezo wake wote kuhakikisha kwamba maandamano ya Azimio yaliyopangwa kufanyika Jumanne wiki ijayo, hayataathiri shughuli zozote.

 

Akizungumza mjini Malava kaunti ya Kakamega siku ya Jumamosi, Rais Ruto alisisitiza kuwa aliwasiliana na kinara wa Azimio Raila Odinga katika juhudi za kutafuta suluhu la amani kumaliza mzozo unaoendelea kati ya upinzani na serikali yake.

 

Kulingana na Ruto, viongozi hao wanatumia maandamano kushinikiza kuingia serikalini.

 

Azimio ilitishia kuanzisha tena maandamano hayo kwa madai kuwa muungano wa Kenya Kwanza ulishindwa kujitolea kufanya mazungumzo yenye manufaa ya pande mbili.

 

Akiwahutubia wafuasi wake huko Kibera baada ya kurejea kutoka ziara ya wiki moja Dubai, Raila alisema maandamano dhidi ya serikali yataendelea kama ilivyopangwa.

 

Aliongeza kuwa maandamano hayo ya amani yatafanyika katika mitaa ya Moi Avenue, Kenyatta Avenue, Haile Selassie Avenue, na Harambee Avenue.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!