Katibu Muthoni Awataka Wakenya Kununua Samani Kutoka Magerezani
Katibu Mkuu wa Idara ya Huduma za Urekebishaji Mary Muthoni ametoa wito kwa Wakenya kununua bidhaa za samani yaani (FURNITURE) zinazotengenezwa na wafungwa kama njia ya kusaidia mpango wa urekebishaji unaoendeshwa na magereza.
Muthoni amesema magereza yanaendesha mojawapo ya sekta imara zaidi za useremala nchini ambayo huzalisha samani za hali ya juu na kuwataka wananchi kutembelea kituo chochote cha kurekebisha tabia na kununua vifaa hivyo.
Akizungumza alipohitimisha ziara ya siku mbili katika magereza ya kaunti za Machakos, Nairobi na Kitui katika magereza makuu ya Machakos, Muthoni amesema pesa zitakazopatikana zitatumiwa ili kununua malighafi ya kuwafunza wafungwa hao.
Pia ametoa wito wa Utatuzi Mbadala wa Migogoro (A.D.R) kama njia ya kusuluhisha mizozo na akasema idara ya serikali itashirikiana na wasimamizi wa serikali ya kitaifa ili A.D.R ifanikiwe.
Kuhusu upanzi wa miti, katibu huyo amefichua kuwa idara ya serikali tayari imepanda miti milioni 1 kama sehemu ya mpango kabambe wa serikali wa kupanda miti bilioni 15 ifikapo 2032.