Ruto, Faki Kutafuta Suluhu La Kudumu La Machafuko Ya Sudan
Rais William Ruto na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki wameafikiana kufanya kazi pamoja kusukuma mbele suluhu la kudumu la ukosefu wa utulivu uliopo nchini Sudan.
Katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu ya Nairobi, Ruto amebainisha kuwa juhudi za Umoja wa Afrika katika kuzuia, kudhibiti na kutatua migogoro katika Bara la Afrika ni za kupongezwa.
Kauli hiyo ya Rais inajiri muda mfupi baada ya mirengo hasimu ya jeshi la Sudan kukubaliana kusitisha vita wa siku tatu, muda mfupi kabla haujakamilika.
Kuongezwa kwa muda kwa saa nyingine 72 – kunafuatia juhudi kubwa za kidiplomasia za nchi jirani, pamoja na Marekani, Uingereza na Umoja wa Mataifa.
Lakini kuna ripoti zinazoendelea za mapigano makali katika mji mkuu Khartoum.
Makubaliano ya hapo awali yaliruhusu maelfu ya watu kujaribu kukimbilia usalama, huku mataifa kadhaa yakijaribu kuwahamisha raia wao.
Takriban wiki mbili za mapigano kati ya jeshi na kundi pinzani la wanamgambo yamesababisha mamia ya watu kupoteza maisha.
Usitishaji mapigano ulitarajiwa kuisha usiku wa manane kwa saa za hapa nchini.