Mwanaume Adungwa Kisu Hadi Kufa Kitengela
Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) huko Kitengela wanachunguza kisa ambapo kijana wa umri wa miaka 20 aliuawa kwa kudungwa kisu na watu wasiojulikana Alhamisi usiku.
Wageni waliokuwa wakiendesha pikipiki baadaye waliutupa mwili wake katika kitengo cha dharura cha Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kitengela.
Kwa mujibu wa taarifa ya hospitali hiyo, watu watatu wa umri wa makamo ambao majina yao hayajafahamika walimchukua marehemu aliyekuwa akivuja damu nyingi na kumpeleka hospitalini hapo majira ya saa tisa alasiri na kumweka kwenye kiti cha magurudumu kwenye wodi ya wagonjwa wa dharura na kutokomea bila kuzungumza na mtu yeyote.
Madaktari katika kituo hicho waligundua kuwa mgonjwa alikuwa amekufa wakati akijaribu kutoa huduma ya kwanza.
Mwili wake ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha kituo hicho baada ya wasimamizi wa hospitali hiyo kuwaarifu polisi.
Marehemu alikuwa amepata jeraha moja la kisu upande wa kushoto chini ya mbavu.
Marehemu aliyetambulika kwa jina la Kapendo, alikuwa akifanya kazi katika eneo la kuponda mawe kando ya Barabara ya Nkuruka.
Leo hii Ijumaa asubuhi, wapelelezi wa Kitengela wagundua eneo la uhalifu katika Norkopir Estate karibu na Kanisa la PCEA.
DCI wa Kitengela Benson Mutie aliambia wanahabari kuwa mshukiwa amekamatwa katika kile kinachoshukiwa kuwa uhalifu wa mapenzi.
Katika wiki moja iliyopita, mji wa Kitengela umekuwa kwenye habari kwa msururu wa mauaji ya kutisha.
Ijumaa iliyopita, mfanyakazi wa Pizza Inn mwenye umri wa miaka 22 aliuawa kwa kuchomwa kisu na mwenzake katika kile kinachoshukiwa kuwa kisa cha mapenzi kupita kiasi.
Siku ya Jumapili usiku, mama mwenye umri wa miaka 24 alimchinja bintiye wa miaka miwili na kumla viungo vyake vya ndani katika mauaji ya kutisha yaliyorekodiwa kwenye kamera za simu na majirani na ambayo yamewashangaza Wakenya.