Home » Hali ya Sintofahamu Kwa Familia Ya Rodgers Aliyeaga Finland

Hali ya Sintofahamu Kwa Familia Ya Rodgers Aliyeaga Finland

Familia ya Rodgers Kipruto, mwanafunzi Mkenya aliyejitoa uhai nchini Finland, iko katika hali ya uchungu baada ya mamlaka husika kuwajulisha wachukue mwili wake ndani ya siku 21, au mwili wake utupwe kwa mujibu wa sheria za Finland.

 

Hali hiyo imejitokeza wakati ambapo familia hiyo ikipitia changamoto mbalimbali huku wazazi wa mwanafunzi huyo aliyesemekana kuwa na msongo wa mawazo, wakitoa wito kwa watu wema kusaidia kuchangisha KSh 4M zinazohitajika kurudisha mwili wake nyumbani kwa mazishi.

 

Kipruto alikuwa miongoni mwa wanafunzi 202 kutoka Kaunti ya Uasin Gishu walioenda Finland kwa mpango  wa masomo kati ya serikali ya kaunti ya Uasin Gishu na vyuo vikuu vitatu ambao ulikumbwa na utata.

 

Wanafunzi hao walijiunga na vyuo vikuu vya Laurea, Jyvaskylla, na Tampere nchini Finland baada ya wazazi kuweka pesa kwenye akaunti ya kaunti, lakini miezi kadhaa baadaye, taasisi hizo zilitaka walipwe karo la sivyo wanafunzi hao wafurushwe.

 

Kamati ya bunge la kaunti iliyochunguza ulaghai huo ilipendekeza uchunguzi ufanyike kuhusu usimamizi wa akaunti ya elimu ya ng’ambo kwa kughushi, matumizi mabaya ya ofisi na ukosefu wa uadilifu.

 

Kipruto alikuwa amekataa tama kutokana na hali hiyo tangu Oktoba mwaka jana na alilalamika kuhusu hali ngumu nchini Finland baada ya kuondoka Kenya Oktoba 30, 2022. Alikuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Laurea, akisomea shahada ya uuguzi baada ya kuacha kazi yake ya uuguzi katika kaunti ya Nakuru.

 

Babake Kipruto, Jonathan Kosgey, aliambia wanahabari kwamba familia hiyo haikuweza kurejesha mwili wake kwa mazishi na wameandaa siku ya kuchangisha fedha ambapo itakuwa ni siku ya Ijumaa.

 

Kosgey alisema ubalozi wa Kenya nchini Finland tayari umewasiliana na familia hiyo na unasaidia kushughulikia masuala ya vifaa ili kuhakikisha mwili huo unaletwa kwa wakati.

 

“Tuna jamaa nchini Uswidi ambao sasa wako Finland kutusaidia na tayari uchunguzi wa maiti unaendelea na tunasubiri ripoti hiyo. Kama familia, tuna matumaini kwamba tutaupokea mwili huo huko JKIA kwa sababu tayari ubalozi wa Finland umetuuliza sisi kwa maelezo ili sisi ndio tuwe tunaupokea mwili huo Nairobi,” alisema.

 

Baba huyo aliyefadhaika aliwasihi wazazi wengine ambao watoto wao bado wanasoma nchini Finland wawe karibu nao ili kuepusha hali tete kama hiyo.

 

Aidha Kosgey alisema familia hiyo imepokea shukrani na rambirambi kutoka kwa Wakenya kutoka tabaka mbalimbali ambao wamekuwa wakimiminika katika eneo lao la Chirchir lililoko Kesses, Kaunti ya Uasin Gishu.

 

Kufuatia masaibu hayo, viongozi katika eneo la Uasin Gishu wanaendelea kushinikiza serikali kukashifu mpango huo wa masomo, wakisema kuwa umewasababishia wanafunzi hao zaidi ya 200 mateso yasiyoelezeka.

 

Ufichuzi wa wanafunzi wa Kenya waliohuzunika nchini Finland baada ya kuachwa katika mpango tata wa masomo uliobuniwa na serikali ya Uasin Gishu umejitokeza kufuatia kifo cha mmoja wao kujiua wiki jana.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!