Waziri Kindiki Alaani Mauaji Ya Shakahola
Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki ametoa wito wa kuwekwa sheria kali kuhusu vituo vyote vya kidini huku maafisa wa upelelezi kutoka Idara ya Upelelezi na makosa ya Jinai (DCI) wakifichua maelezo zaidi ya kutatiza kuhusu kanisa la Good News International Church huko Malindi, Kaunti ya Kilifi.
Waziri Ameyasema hayo alipokuwa akilaani visa vya miili kufukuliwa kule Shakahola, ambavyo vimesababisha kupatikana kwa miili 39.
Waziri wa Mambo ya Ndani pia ameamuru kuimarishwa kwa wanajeshi wa polisi katika eneo la Shakahola kusaidia katika uchunguzi unaoendelea kabla ya ziara yake siku ya Jumanne wiki ijayo.
Uchunguzi huo ulichochewa baada ya wafuasi wachache wa dini hiyo kuokolewa na maafisa kutoka kituo cha polisi cha Malindi, na baadaye wanafamilia wa waathiriwa wengine waliotoweka kukusanyika katika kituo cha polisi kwa matumaini ya kuwapata jamaa zao.
Mshukiwa mkuu ni mhubiri wa kanisa hilo, Paul Mackenzie Nthenge, ambaye anadaiwa kuwalaghai waumini kufunga “ili wamwone Mungu,” tambiko lililosababisha vifo vya waumini wengi.
Hakimu Olga Onalo wa Mahakama Kuu ya Malindi alimpa Mackenzie dhamana ya Ksh.10,000 uchunguzi ukiendelea awali.
Hata hivyo, bado hajafunguliwa mashtaka kwa sababu mtaalamu wa serikali na maafisa wa DCI bado hawajafukua miili yote.