Azimio Kuanzisha Maandamano Dhidi Ya Serikali Wiki Ijayo
Muungano wa Azimio umetangaza kuwa maandamano dhidi ya serikali yataanza tena wiki ijayo baada ya mapumziko ya mwezi mmoja.
Naibu kiongozi wa chama cha ODM Wycliffe Oparanya amesema kuwa maandamano yataanza Mei 2.
Wiki iliyopita, kiongozi wa Azimio Raila Odinga alitangaza kwamba watarejelea maandamano baada ya kile alichosema ni kushindwa kwa serikali kuchukulia kwa uzito mazungumzo ya pande mbili.
Kufuatia mikutano ya mashauriano na viongozi wengine wa Azimio, wanaazimia kuwa na mazungumzo na maandamano sambamba.
Muungano huo ukijibu tamko la Baraza la Maaskofu linaloitaka serikali kuingilia kati na kupunguza gharama ya bidhaa za kimsingi nchini, Azimio imeeleza kuwa tayari kushirikiana nao katika kufuatilia suala hili kwa ajili ya Wakenya wanaoteseka.
Katika taarifa ya kurasa sita, Maaskofu pia wanaeleza kutokubali kwao maandamano haribifu na kutetea mazungumzo, ambayo wanasema ndiyo njia pekee ya kiraia kutatua changamoto za kijamii na kisiasa za Kenya.
Hata hivyo, upinzani haukubaliani na uamuzi wa kanisa kutangaza maandamano hayo kuwa ya vurugu, kinyume na katiba.
Upinzani sasa unaliomba kanisa kushirikiana na Wakenya katika kutoa wito kwa Serikali kuheshimu kifungu cha 37 cha Katiba, ambacho kinampa kila mtu haki ya kukusanyika kwa amani na kupiga kura.
Mazungumzo ya pande mbili yalianza wiki iliyopita huku viongozi wa Azimo na Kenya Kwanza wakikubaliana kuhusu eneo la mkutano.
Ingawa kumekuwa na hatua tofauti bado suluhu kuhusu muundo wa kamati ya dharura.
Kenya Kwanza inapinga kujumuishwa kwa Mbunge wa Pokot Kusini David P’Kosing wa chama cha (KUP) kama mwanachama wa timu ya Azimio kwa misingi kwamba kiongozi wa chama chake John Lonyangapuo ameingia katika muungano wa Kenya kwanza.
Kwa upande mwingine Azimio imepinga kujumuishwa kwa mbunge wa Eldas Adan Keynan katika timu ya Kenya Kwanza ikisema kuwa Jubilee inahusishwa na Azimio.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah alisema kuondolewa kwa jina lolote kwenye orodha lazima kupelekwe kwa uongozi na vyombo husika vya chama.