Barasa La Mawaziri Laagiza NTSA Kuanza Ukaguzi Wa Magari
Baraza la Mawaziri likiongozwa na Rais William Ruto limeibua wasiwasi kuhusu ongezeko la visa vya ajali za barabarani kote nchini.
Baraza hilo limehusisha ongezeko la visa vya ajali za barabarani na mapuuza ya wakenya kwenye barabara kuu nchini.
Ili kurejesha hali usalama barabarani, baraza hilo limeagiza Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) kuongeza ufuatiliaji dhidi ya madereva wanaokiuka sheria za trafiki.
Agizo la Baraza la Mawaziri limejiri kufuatia ajali iliyohusisha gari la wafanyakazi wa umma na lori katika Barabara Kuu ya Nairobi-Nakuru leo jana jumanne.
Taarifa za awali zilieleza kuwa wanafunzi watano waliangamia kufuatia ajali hiyo. Wanafunzi hao walikuwa wakielekea Nairobi wakati wa ajali hiyo mbaya.
Takriban wanafunzi wengine saba walipata majeraha kufuatia ajali hiyo.
Mnamo Jumatatu, Aprili 17, watu wanne walithibitishwa kufariki baada ya basi la Tahmeed kubingiria kwenye barabara kuu ya Nakuru- Eldoret.
Mnamo Aprili Jumamosi, 15, watu kumi walifariki baada ya basi moja kupoteza mwelekeo na kubingiria katika eneo la Josa kando ya barabara ya Wundanyi-Mwatate katika Kaunti ya Taita Taveta.
Kufuatia kukithiri kwa ajali, washikadau wengine wameitaka NTSA kurekebisha mamlaka yake ya ukaguzi wa magari ili kuruhusu magari yanayofaa barabara pekee katika barabara kuu za Kenya.
Katika mahojiano na wanahabari Edward Gitonga na mwenyekiti wa Chama cha Usalama Barabarani, amedokeza kuwa baadhi ya magari ya umma yalikuwa yakishirikiana na maafisa wa NTSA kupata vyeti vya ukaguzi.
Kwa upande mwingine, David Kiarie Njoroge, mwenyekiti wa Chama cha Usalama Barabarani nchini Kenya, ametoa wito kwa NTSA kuweka sheria za lazima za kubandika vyeti vya ukaguzi kwenye magari yote ya umma.