Bei Ya Unga Imeshuka – Msemaji Wa Ikulu
Serikali inasema bei ya unga wa mahindi imeanza kushuka, hali inayoashiria afueni kwa gharama ya juu ya maisha inayoathiri Wakenya wengi.
Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed amesema kwamba gharama ya pakiti ya kilo 2 ya Unga imeshuka hadi Kshilingi mia 159 na mia 160, kulingana na wasagaji kote nchini.
Mohamed amebainisha kuwa kushuka kwa bei hizo kunafuatia ahadi ya Rais William Ruto wikendi kwamba gharama ya bidhaa hiyo itashuka pakubwa kuanzia wiki hii.
Kulingana na Mohamed, pakiti ya kilo 2 ya Unga ilikuwa ikiuzwa kwa takriban Kshilingi mia 230, wakati utawala wa Kenya Kwanza ulipochukua hatamu.
Rais William Ruto Ijumaa alisema serikali imejitolea kushughulikia gharama ya juu ya maisha nchini.
Akizungumza huko Mavoko katika Kaunti ya Machakos, ambapo alizindua mradi wa maji wa Ksh2.7 bilioni, Ruto alifichua kuwa bei ya Unga itashuka baada ya kuwasili kwa mahindi kutoka nje.
Gharama ya Unga ilipanda zaidi mwaka jana baada ya Rais Ruto kufutilia mbali ruzuku zilizowekwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Licha ya madai kutoka kwa upinzani, Ruto alisema utawala wake utawekeza kwa wazalishaji, akitaja ruzuku kama matumizi sio endelevu.