Home » Takriban Wakenya 3,000 Wamekwama Nchini Sudan – Alfred Mutua

Takriban Wakenya 3,000 Wamekwama Nchini Sudan – Alfred Mutua

Waziri wa Masuala ya Kigeni Alfred Mutua amesema kuwa takriban Wakenya elfu 3,000 wamekwama nchini Sudan kutokana na ghasia zinazozidi kuongezeka.

 

Kulingana na Mutua, Wakenya nchini Sudan wamelazimika kujifungia ndani ya nyumba zao na kutafuta usaidizi wa kurejea nchini.

 

Akizungumza katika hafla ya kutoa shukrani za serikali huko Machakos jana Jumapili, Mutua alisema kuwa mipango ya kuwasafirisha raia hao kurudi nyumbani inaendelea na tayari wako kwenye mazungumzo na shirika la ndege la Kenya Airways ambao wako tayari.

 

Mutua aliendelea kuwataka raia wa Kenya kujiandikisha kila mara kwa balozi katika mataifa husika, kwani inasaidia katika mawasiliano rahisi na kuitikia machafuko yanapozuka.
Wanajeshi wa Sudan, siku ya Jumamosi, walijihusisha na vurugu za kutaka mamlaka na Wanajeshi wa Rapid Support Forces (RSF).

 

RSF ilidai udhibiti kamili wa ikulu ya rais hata kama jeshi lilidai udhibiti wa viwanja vyote vya ndege.

 

Kwa upande wake….Rais William Ruto ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu mzozo unaoendelea huku akitoa wito kwa pande zote zinazohusika na ghasia za kijeshi kushughulikia tofauti hizo kwa njia za amani.

 

Jana Jumapili, wakati wa mkutano na jumuiya ya Maendeleo (IGAD), Rais Ruto alitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama kati ya pande zinazozozana nchini Sudan.

 

Waliokuwa katika kikao hicho cha dharura ni Marais Salva Kiir wa (Sudan Kusini), Yoweri Museveni wa (Uganda), Ismail Omar Guelleh wa (Djibouti) na Hassan Sheikh Mohamud wa (Somalia).

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!