Home » Polisi Wamtafuta Askofu Aliyechoma Fuvu La Kichwa Cha Binadamu Homa Bay

Polisi Wamtafuta Askofu Aliyechoma Fuvu La Kichwa Cha Binadamu Homa Bay

Polisi katika Kaunti ya Homa Bay wanamsaka Askofu anayedaiwa kuchoma fuvu la kichwa cha binadamu kule Lwanda Nyamasare, eneo bunge la Suba Kaskazini jana jioni.

 

Kasisi huyo ambaye amejificha aliwaongoza waumini wa kanisa lake hadi ufukweni ambako alidai kuwa alielekezwa na Mungu kwenda kutoa fuvu la kichwa cha binadamu kwenye maji ya Ziwa Victoria ndani ya ufukwe wa Lwanda Nyamasare kabla ya kulichoma moto mara baada ya kufukuliwa.

 

Kulingana na ripoti ya polisi, askofu huyo alikuwa amealikwa kwa sala ya Pasaka katika kanisa la eneo la Gembe Magharibi siku ya Jumamosi.

 

Akiwa kanisani hapo, askofu huyo alidai kuwa alipata maono wakati wa maombi ya kutafuta fuvu la kichwa kwenye maji ya Ziwa Victoria na kuwaambia waumini kuhusu maono hayo na kuwashawishi wamfuate hadi ziwani ambako alilitoa fuvu la kichwa cha binadamu kutoka kwenye maji.

 

Kwa mujibu wa Msaidizi wa chifu wa Kitongoji cha Kasgunga Mashariki Francis Kasuku, suala hilo liliripotiwa kwake na mwenyekiti wa Lwanda Nyamasare Beach Michael Aroko baada ya askofu huyo na waumini wake kuanza shughuli hiyo.

 

Msimamizi huyo alitoa taarifa kwa maafisa wa polisi lakini hadi maafisa hao walipofika katika ufuo huo, askofu huyo alikuwa ametoweka kusikojulikana na juhudi za kumtafuta hazikufanikiwa.

 

Katika harakati za uchunguzi, maafisa wa polisi wa Kituo cha Polisi cha Mbita walipeleka fuvu hilo katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay ambapo walithibitisha kuwa ni fuvu la kichwa cha binadamu.

 

Kwa sasa, fuvu hilo limehifadhiwa katika chumba cha maiti likisubiri uchunguzi wa kitaalamu.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!