Jalang’o: Ikiwa Raila Hatakuwa Rais Basi Nitakuwa Rais Wa Kwanza Kutoka Luo
Mbunge wa Lang’ata Felix Odiwuor, almarufu Jalang’o, amesisitiza kuwa atakodolea macho kiti cha Urais katika siku zijazo za safari yake ya kisiasa.
Kulingana na Jalang’o, analenga kuweka historia ya kuwa rais wa kwanza kutoka eneo la Luo ikiwa Raila Odinga atashindwa kunyakua kiti hicho katika uchaguzi ujao unaotarajiwa kufanyika 2027.
“Jambo moja ninalojua ni kwamba siku moja, na nimeanza kutumia hashtag IpoSiku, ikiwa Baba hatakuwa rais nitakuwa rais wa kwanza wa Luo.Ninachoomba ni uzima tu. Siku utakapoona bango langu, Jalang’o akigombea urais, nitakuwa Amri Jeshi Mkuu.”
Mbunge huyo alidokeza kwamba, kabla ya nafasi ya juu ya taifa, yuko tayari kuchunguza nyadhifa tofauti za uchaguzi katika safari yake ya kisiasa inayoonekana.
Vile vile alizua mzozo kati yake na Raila kuhusu utiifu wake kwa Rais William Ruto, akisema kuwa yuko tayari kuadhibiwa na kupachikwa majina maadamu atatoa ahadi zake kwa wawakilishi wa Lang’ata.
Jalang’o aliongeza kuwa hafai kuitwa msaliti na chama cha Orange Democratic Movement (ODM), akisema uaminifu wake kwa Raila hauwezi kupingwa lakini hilo haliwezi kumzuia kufanya kazi na serikali.
“Penzi langu kwa Baba haliwezi kubadilika, anajua, nilikutana naye tangu siku hiyo na pia nimempigia simu. Hafurahii ila dhamiri yangu ni kutoa kwa watu na iwe hivyo.”