Home » Gachagua Akiri Serikali Ina Changamoto Kulipa Mishahara

Gachagua Akiri Serikali Ina Changamoto Kulipa Mishahara

Naibu Rais Rigathi Gachagua amethibitisha ripoti kuwa serikali ina changamoto katika kulipa mishahara ya wafanyikazi wa umma.

 

Akizungumza wakati wa ibada katika eneo bunge la Mathira Jumapili, Naibu Rais amesema changamoto za kifedha nchini pia zimeathiri kaunti mablimbali.

 

“Ni kweli tuna changamoto katika kulipa mishahara, kutoa pesa kwa magavana. Kwa sababu serikali ya kupeana mikono iliharibu nchi hii, walikopa pesa kushoto kulia na katikati. Kwa sababu sisi ni serikali inayowajibika, tunapaswa kulipa fedha hizi,” alisema.

 

Gachagua aliongeza kuwa baadhi ya mikopo ya serikali ilikuwa imeiva wiki jana, hivyo kuilazimu kulipa deni hilo.

 

“Tulichokusanya wiki mbili zilizopita kilitosha kulipa mikopo. Tunachokusanya wiki hii kitalipa mishahara na mahitaji mengine,” aliongeza.

 

Gachagua alitetea serikali ya Rais William Ruto, akisema imelazimika kujenga upya kila kitu tangu mwanzo kwani pesa ziliibwa wakati wa utawala wa Rais wa zamani Uhuru Kenyatta.

 

“Tuko katika hali ngumu, si sisi tuliokopa fedha hizo bali tunalazimika kulipa kwa sababu inadaiwa na Kenya. William Ruto hawezi kukimbia madeni hayo ingawa hakuyapata,” Gachagua aliwaambia waumini katika mji aliozaliwa.

 

Wabunge ni miongoni mwa watumishi wa umma ambao hawajapata mishahara yao ya Machi kutokana na mzozo wa fedha.

 

Haya, Mwenyekiti wa Baraza la Washauri wa Kiuchumi la Rais William Ruto, David Ndii pia alisema ni matokeo ya deni kubwa la nchi.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!