Mwili Wa Mwanamke,108, Uliozikwa Kimakosa Wafukuliwa
Mwili wa mwanamke mwenye umri wa miaka 108 umefukuliwa leo Alhamisi katika eneo la Kandara eneo la Kibiku katika hali ambayo imeibuka kuwa ya kutatanisha ya utambulisho usio sahihi.
Shughuli ya kufukuliwa kwa mwili wa Elizabeth Wairimu iliongozwa na Maafisa wa Afya na kuhudhuriwa na familia kutoka pande zote mbili.
Kulingana na mjukuu wa Lydia Muthoni, James Mungai, wakati wa maziko wiki jana, familia iliuchukua mwili wa Wairimu kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Gaichanjiru ikidhani ni wa Lydia Muthoni, 78.
Mungai ameambia wahandishi wa habari kuwa siku ya kuhamisha mwili walipokwenda katika chumba cha kuhifadhia maiti na kuonyeshwa mwili wa marehemu Wairimu, waliamini walikuwa ni mwili sahihi na kuhusisha mabadiliko hayo na kuharibika baada ya kifo.
Mungai anadai alipokea simu kutoka kwa shangazi yake Jumanne akimjulisha kuwa walizika maiti isiyofaa na kwamba uchimbaji wa kaburi ulikuwa karibu.
Kulingana na Mungai, familia hizo mbili zilikutana kortini jana Jumatano ili kutatua mkanganyiko huo na kuafikiana kuhusu uchimbaji wa kaburi hilo.
Huku hayo yakijiri, familia ya Wairimu, ambayo bado inakumbwa na kisa hicho cha ajabu, imetangaza kwamba mipango ya kumzika jamaa yao mwenye umri wa miaka 108 iko mbioni.
Kulingana na mwanafamilia John Mwangi, waligundua mkanganyiko huo Aprili 4 walipokuwa wakienda kuchukua mpendwa wao wa familia.
Familia hizo mbili zimeelezea matumaini yao kwamba chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Misheni ya Gaichanjiru kitarekebisha mkanganyiko huo.
Mwangi amesema kwamba chumba cha kuhifadhi maiti kimekuwa cha msaada tangu tukio hilo kuripotiwa, na kwamba familia zilizolipa Ksh.100,000 na Ksh.80,000 kwa mipango ya mazishi, mtawalia, zitafidiwa.
Mwili wa Wairimu umerejeshwa katika chumba cha kuhifadhia maiti leo Alhamisi kufuatia kufukuliwa kwake.