Mahakama Yakataa Kusitisha Uajiri Wa Mwenyekiti , Makamishna Wa IEBC

Mahakama kuu imekataa kusitisha uajiri unaoendelea wa mwenyekiti na makamishna sita wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na badala yake ikaagiza kwamba kesi hiyo isikizwe baina ya pande zote mnamo Aprili 13, 2023.
Katika kesi hiyo, Seneta wa Busia Okiya Omtatah alikuwa ameelekea mahakamani akitaka kusimamisha shughuli zote za Jopo la Uteuzi ikiwa ni pamoja na uajiri unaoendelea wa mwenyekiti na wanachama wa IEBC.
Seneta Omtatah, katika suala hilo alitaka mahakama kusitisha shughuli ya bunge hadi mabadiliko yafanywe katika muundo wa jopo la uteuzi na tamko kwamba Sheria ya IEBC Na.1 ya 2023 ni kinyume cha katiba.
Iwapo maafisa hao wa IEBC watateuliwa na majina kutumwa kwa Rais William Ruto, Omtatah anataka mahakama kuzuia uteuzi wao hadi kuamuliwa kwa kesi hiyo.