Home » NCIC Yawapongeza Ruto, Raila Kwa Makubaliano Ya Mazungumzo

Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imewapongeza Rais William Ruto na kinara wa upinzani Raila Odinga kwa kukubali kufanya mazungumzo na kujadili masuala ambayo upinzani unapendekeza dhidi ya serikali.

 

Mwenyekiti wa NCIC Samuel Kobia, katika taarifa, ametaja uamuzi wa wanasiasa hao wawili kuwa muhimu wa “utamaduni na uongozi wa busara”.

 

Kutokana na hilo, Kobia amesema NCIC itakuwa ikiitisha msururu wa mazungumzo ya kitaifa kuhusu ustawi wa kiuchumi, uthabiti wa kisiasa na uwiano wa kijamii nchini Kenya.

 

Siku ya Jumapili, Odinga alisitisha maandamano ya kila wiki ya kupinga serikali aliyokuwa ameandaa kwa wiki mbili na kusema yuko tayari kwa mazungumzo kushughulikia masuala muhimu ambayo upinzani una nayo na serikali ya Ruto.

 

Ilifuatia ombi la Rais Ruto kwa Odinga saa chache kabla, akimtaka kusitisha maandamano na badala yake afikirie mazungumzo kuhusu mchakato wa wabunge wa pande mbili za kuwaajiri makamishna katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

 

Kuundwa kwa chombo kipya cha uchaguzi ni mojawapo ya masuala ambayo upinzani ulikuwa umeibua kuhusu utawala wa Rais Ruto.

 

NCIC ilikuwa miongoni mwa tume iliyokashifu maandamano ya Odinga. Kobia wiki jana alielezea wasiwasi wake kwamba maandamano hayo yanazua mvutano kote nchini, akisema wana wasiwasi kwamba vitendo kama hivyo vitaongezeka na kuwa mivutano ya kikabila na pia matamshi ya chuki.

 

Alitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa maandamano hayo na kuwataka Ruto na Odinga kuketi na kutatua masuala yao.

 

Wakati huo huo Odinga amesema yuko tayari kuanza mazungumzo na Mkuu wa Nchi, lakini hata hivyo, alitishia kuanzisha tena maandamano ikiwa matokeo ya mazungumzo yatakosa maana yatakayoafikiwa ndani ya wiki moja.

 

Yakijiri hayo… Viongozi wa kidini sasa wanashinikiza mazungumzo kati ya serikali na upinzani ambayo yameratibiwa kufanyika kupitia bunge kujumuisha wadau zaidi badala ya wanasiasa pekee.

 

Viongozi hao wanataka wanataka mashirika yasiyo ya serikali, viongozi wa kidini na mashirika ya kijamii kuhusishwa ili mafikiano yadhihirishe ujumuishwaji wa wakenya.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!