Waziri Eliud Owalo Alaani Maandamano Huko Migori
Waziri wa teknolojia na mawasiliano Eliud Owalo amewataka wakazi wa Nyanza kutojihusisha na maandamano yanayoendelea yanayoitishwa na kiongozi wa Muungano wa Azimio-One Kenya, Raila Odinga.
Akizungumza huko Migori wakati wa zoezi la usambazaji wa chakula katika eneo la Nyarongai eneo bunge la Suna Mashariki, Waziri Owalo amesema Rais William Ruto ana nia njema na wenyeji wa Nyanza kwani tayari amewateua viongozi mbalimbali kutoka eneo hilo, kwa nia ya kuendeleza eneo hilo kiuchumi.
Waziri huyo amesema kuwa utawala wa Kenya Kwanza kulingana na manifesto yake na uongozi wa Rais Ruto uko tayari kufanya kazi na Wakenya wote kote nchini licha ya uungwaji mkono mdogo wa kisiasa aliopata.
Aidha, Owalo amepuuzilia mbali wazo la maandamano ya kisiasa akisema muda wa uchaguzi umepita, na kwamba maandamano hayo yanawafanya wawekezaji kukaa mbali na kenya, na vile vile yanasababisha uharibifu wa biashara, na kuhatarisha mustakabali na maisha ya vijana.
Owalo ameandamana na kundi la viongozi akiwemo Katibu Mkuu wa Utawala wa Barabara Nicholas Gumbo, Mwenyekiti wa Bodi ya Nyuklia ya Kenya Edick Anyanga na aliyekuwa Mbunge wa Migori John Pesa, miongoni mwa wengine.
Vile vile viongozi hao wamepinga maandamano hayo wakionyesha kuwa maandamano hayo hayatasuluhisha gharama kubwa za maisha nchini bali yataingilia shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi ndani ya mkoa huo.