Rais Ruto Na Raila Odinga Wazidi Kushinikizwa Kuzungumza

Kundi moja la makasisi linalojumuisha zaidi ya makanisa 17 sasa linapendekeza kuwa na mazungumzo ya kitaifa baina ya pande mbili ya kisiasa zinazozana kwa minajili wa mastakabali wa taifa. Makasisi hao aidha wamemuomba kiongozi wa Azimio Raila Odinga kusitisha misururu ya maandamano aliyoitisha kote nchini.
Badala yake, watumishi hao wa mungu wamemtaka Odinga kutumia njia zote ziliwekwa kisheria kutatua mizozo yoyote ama malalamishi aliyonayo.
‘’Ingawa Katiba inahakikisha uhuru wa maandamano na kura, hili si suluhu la changamoto nyingi za kiutawala zinazokabili taifa. Tunawasihi viongozi wetu wa kisiasa kutumia taasisi za kushughulikia changamoto za utawala badala ya maandamano ambayo yanaweza kuzorota na kuleta machafuko’’ wakasema makasisi.
Wanasema ingawaje maandamano inakubalika kikatiba, hatua hiyo imegeuka na kuwa ukumbi wa maafa, wizi, vurugu, uporaji wa mali, uhalifu na aina zingine za utovu wa nidhamu.
Wametoa mfano wa kuchomwa kwa kanisa la PCEA na Msikiti katika kitongoji duni cha Kibera kuwa moja wapo ya mambo yanayotishia amani ya taifa.
Aidha, makasisi hao wanataka polisi kuwa waangalifu wakati wa maandamano na kuepuka kutumia nguvu kupindukia wakati wanawakabili waandamanaji.
Haya yanajiri wakati Odinga amesisitiza maandamano aliyopanga kila siku ya Jumatatu na Ijumaa yataendelea kama yalivyokuwa yamepangwa.