Raila Amlaumu Naibu Rais Gachagua
Kiongozi wa muungano wa Azimio La Umoja One Kenya Raila Odinga amemlaumu Naibu Rais Rigathi Gachagua kufuatia uvamizi wa leo hii Jumatatu wa ardhi inayomilikiwa na familia ya Kenyatta na kiwanda chake cha gesi cha (East Africa Specter Limited) na wahuni.
Watu hao wasiojulikana walivamia ardhi ya Kenyatta iliyo kando ya Barabara ya Nairobi Eastern Bypass, na kukata miti na kuwaondoa kondoo leo hii Jumatatu asubuhi, saa chache baada ya kiwanda cha gesi cha Odinga kushambuliwa na madirisha kadhaa kuvunjwa.
Kulingana na kiongozi huyo wa upinzani, Gachagua aliwafadhili majambazi hao kupigana naye na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, ambaye Naibu Rais amenukuliwa akisema ndiye aliyehusika na maandamano ya Azimio dhidi ya serikali.
Siku ya Jumapili, Odinga alimshutumu naibu rais kwa kuandaa oparesheni kuu ya ghasia dhidi ya maandamano ya Azimio.
Alisema kituo cha kuhifadhia silaha na kamandi kimeanzishwa katika maeneo mawili tofauti, ambayo alidai yana silaha za kila aina, kuanzia bunduki, panga na mapanga.
Katika taarifa iliyosambazwa kwenye Twitter, kiongozi huyo wa upinzani aliendelea kudai kuwa silaha hizo zinasafirishwa hadi maeneo hayo ndani ya gari lililofichwa kama gari la wagonjwa.