Home » Jopokazi Lililobuniwa Kuwatathmini Makamishna Wa IEBC Kuapishwa Leo Alhamisi

Jopokazi Lililobuniwa Kuwatathmini Makamishna Wa IEBC Kuapishwa Leo Alhamisi

Wanachama saba wa jopo la uteuzi lililobuniwa kuongoza shughuli ya kuwaajiri Mwenyekiti na Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wataapishwa alasiri hii.

 

Saba hao wataapishwa na Jaji Mkuu Martha Koome wakati wa hafla itakayofanyika katika Jengo la Mahakama ya Juu.

 

Saba hao ni Bethuel Sugut, Novince Euralia Atieno, Charity s. Kisotu, Evans Misati James, Benson Ngugi Njeri, Nelson Makanda na Fatuma Saman.

 

Jopo hilo linajumuisha wawakilishi kutoka Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), Tume ya Huduma za Bunge, Kamati ya Uhusiano ya Vyama vya Kisiasa (PPLC), Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK), na Baraza la Dini Mbalimbali la Kenya.

 

Rais William Ruto Jumatatu iliyopita aliteua jopo la uteuzi wa wanachama saba kupitia notisi ya gazeti la serikali ya tarehe 27 Februari 2023.
Rais Ruto aliwapa wanachama hao jukumu la kuwateua watu kwa nyadhifa za Uenyekiti na Makamishna wa IEBC.

 

Shughuli ya kuunda tume ya uchaguzi inajiri mwezi mmoja baada ya muda wa Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, Makamishna Abdi Guliye na Boya Molu kukamilika Januari mwaka huu.

 

Makamu Mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera na Makamishna Justus Nyang’aya na Francis Wanderi walijiuzulu mwaka jana kufuatia madai ya ukiukaji wa katiba na utovu mkubwa wa nidhamu wakati wa uchaguzi mkuu uliokuwa na ushindani mkali wa 2022.

 

Irene Masit ambaye ndiye kamishna pekee aliyechagua kusalia alifutwa kazi na Rais Ruto Jumatano kufuatia pendekezo la mahakama iliyokuwa ikiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jaji Aggrey Muchelule iliyochunguza mwenendo wake.

 

Mahakama hiyo iliyowasilisha ripoti yake kwa Rais Ruto Jumatatu iliyopita ilimpata Masit na hatia ya ukiukaji mkubwa wa katiba na sheria na kumtaka Rais William Ruto kumfukuza afisini.

 

Sababu za utovu mkubwa wa nidhamu wa kamishna katika ripoti ya mahakama zilipatikana katika vipengele vitatu, kwamba Masit alikuwa amekiuka sura ya 6 ya Katiba,walikuwa wameshirikiana na mgombea kutoka kundi moja na kwamba alikuwa amekataa matokeo ya Uchaguzi wa Rais wa 2022.

 

Kwa hivyo, Rais Ruto alimfuta kazi Masit kupitia Notisi ya Gazeti ya Machi 1, 2023.

 

Ibara ya 251 (6) ya katiba inamtaka Rais baada ya kupokea ripoti ya mahakama, kuchukua hatua kwa mujibu wa mapendekezo ndani ya siku 30.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!