Watu Watatu Wauawa Katika Shambulizi Jipya Marsabit
Majambazi alfajiri leo Jumatano wamewavamia na kuua watu watatu huko Marsabit.
Wahalifu hao walifanya mashambulizi katika eneo la Hallan, Kargi licha ya vita vilivyoanzishwa upya na serikali dhidi ya ujambazi katika kaunti zilizochaguliwa.
Wavulana wawili wenye umri wa kati ya miaka 5 na 7 na mwanamume wa makamo wamefariki kutokana na uvamizi huo.
Mwanamume mmoja anauguza majeraha mabaya katika shambulio hilo ambalo limewatia wakazi hofu.
Chifu msaidizi wa eneo hilo Moses Galoro amethibitisha kisa hicho na kuongeza kuwa idadi isiyojulikana ya mbuzi na kondoo pia waliibiwa.
Operesheni ya pamoja ya polisi na kijeshi inaendelea katika kaunti za Baringo, Pokot Magharibi, Samburu, Turkana na Elgeyo Marakwet huku Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki akiahidi kurejesha hali ya utulivu katika maeneo yaliyoathiriwa na ujambazi.
Kaunti zingine zinazolengwa ni Lamu, Tana River, Marsabit, Isiolo, na eneo lote la Kaskazini Mashariki chini ya vitisho vya mara kwa mara vya ugaidi na vikundi vya wanamgambo wa Somalia.